Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali inatambua kuna mila zenye faida ambazo zinapaswa kuendelezwa na mila zenye kuleta madhara ikiwemo mila ya kuwekeza mke akiwa tumboni mwa mama.
“Mila hii ina madhara kwa kuwa inachochea ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni na inamnyima mhusika haki yake ya msingi ya kumchagua mwenza wa kuishi naye umri utakapofika.” amesema Dkt. Gwajima
Ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mary Mwinyi aliyehoji Serikali ina mpango gani wa kufuatilia mila potofu za kuwekeza mke akiwa tumboni mwa Mama hasa katika mikoa ya Manyara na Arusha.