Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana amewapongeza waratibu wote na wananchi wa Ngorogoro mkoani Arusha walioamua kuhamia kwa hiari katika kijiji cha Msomera kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga, kwa uratibu mzuri wa watu na mifugo yao hali iliyofanikisha wafike salama.
Dkt Chana ameyasema hayo katika kijiji cha Msomera baada ya kujihakikishia kuwa mifugo ya wafugaji hao kutoka Ngorogoro imefika salama.
“Tunamshuku Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Makamu wetu wa Rais Dkt. Philip Mpango pamoja na Waziri Mkuu wetu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kutuongoza vema kwenye jambo hili, limeenda vizuri na linaenda vizuri kwa wana Ngorogoro wenyewe kuhama kwa hiari, sisi kama wizara tutaendelea kutekeleza maagizo ya viongozi wetu wa juu ili kuhakikisha ndugu zetu wanaishi kwenye mazingira bora kama mlivyoyaona.” amesema Waziri Chana
Akizungumzia hali ya usalama ya wafugaji hao, mkuu wa mkoa wa Tanga Adam Malima amesema, wanachi hao wapo salama na wataendelea kuwa salama wao na mifugo yao
Amesema mkoa wa Tanga umejipanga vema kuwahudumia vizuri kwa kuwa wameishakuwa wakazi wa mkoa humo.
Naye Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema miradi ya maji imeishafanyika na wanaendelea kuhakikisha hakutokuwa na changamoto yeyote ya maji kwa matumizi ya binadamu na ya kunywesha mifugo iliyofika na itakayofika.