Dkt. Abbasi aelezea utoaji wa vitambulisho (press card) kwa wanahabari wanafunzi

0
360

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 na Kanuni zake za 2017, 18(1) inaruhusu wanafunzi wa taaluma ya habari kupata vitambulisho vya wanahabari.

Dkt. Abbasi amesema hayo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu kanuni mpya za maudhui na kuongeza kuwa vitambulisho hivyo vitawasaidia wasipate shida na wafanye kazi kwa weledi wakati wakiwa katika mafunzo kwa vitendo.

Akizungumzia sekta ya michezo iliyochini ya wizara yake, Dkt. Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa wajibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) unapaswa kuwa mkubwa kuliko sasa.

“Ni lazima uwepo mifumo inayohakikisha inakomesha masuala ya ujanja ujanja kwenye usajili pamoja na masuala ya kuingiza wachezaji wa kigeni yanakaa vizuri,” amesema Abbasi.

Kauli hiyo imekuja wakati klabu za Simba na Yanga zikivutana kuhusu usajili wa mchezaji Bernard Morrison ambapo kila klabu inadai kuwa ni mchezaji wake halali. Sakati hilo lipo mikononi mwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambao wanaendelea kulitafutia ufumbuzi.