Rais John Magufuli amemteua na kumuapisha Kamishna Diwani Athuman kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema kuwa uteuzi wa Kamishna Diwani umeanza hii leo na hafla ya kumuapisha imefanyika hii leo jijini Dar es salaam.
Kabla ya uteuzi huo Kamishna Diwani Athuman alikua Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU).
Akizungumza baada ya kumuapisha Kamishna Diwani, Rais Magufuli amemtaka kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kuweka mbele maslahi ya Taifa.
Kamishna Diwani Athuman anachukua nafasi ya Dkt Modestus Kipilimba ambaye atapangiwa kazi nyingine.