Diwani ‘aliyepotea’ apatikana kwa Ashura

0
98

Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam wamefanikiwa kumpata diwani wa kata Kawe kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mutta Rwakatare aliyekuwa akitafutwa na ndugu zake kuanzia mwezi Februari mwaka huu.

Taarifa za kupatikana kwa diwani huyo zimetolewa na Kamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne.

Kamanda Muliro amesema baada ya uchunguzi walifanikiwa kumpata Mutta tarehe 23 mwezi huu maeneo ya Tabata akiwa katika nyumba ya mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Ashura ambaye amedai ni rafiki yake wa siku nyingi.

Amesema Mutta mwenye umri wa miaka 43 anadaiwa kufika nyumbani kwa Ashura tarehe 19 mwezi huu akiwa katika hali ya ulevi uliopindukia.

Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam wamefanikiwa kumpata diwani huyo wa Kawe ambaye ni mtoto wa Marehemu Dkt. Getrude Rwakatare zikiwa zimepita siku chache baada ya Meya wa Kinondoni, Songoro Mnyonge kuviomba vyombo vya dola na waandishi wa habari kusaidia kumtafuta diwani huyo ambaye kutoonekana kwake kunawanyima fursa wananchi waliomchagua ya kuwatumikia.