Dhamana kwa aliyekuwa Rais wa Simba SC Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange (Kaburu) imeshindwa kupatikana kufuatia Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kuwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama kuondoa mashtaka ya utakatishaji fedha katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.
Hatua hiyo imekuja wakati Washtakiwa hao walipopandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba kwa ajili ya kukamilisha masharti ya dhamana ili waweze kuachiwa huru na kujitetea.
Upande wa Mashtaka umedai kuwa, DPP amewasilisha kusudio la kukata rufaa kutokana na uamuzi wa Mahakama hiyo uliotolewa hapo jana wa kuyaondoa Mashtaka mawili ya utakatishaji fedha baada ya kuona kuwa hawana kesi ya kujibu.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi Nehemia Nkoko ameiomba Mahakama kuendelea na zoezi la kuwapatia dhamana wateja wake, kwa kuwa upande wa Mashtaka jana ulipoulizwa kama unapingamizi lolote juu ya Washtakiwa kupewa dhamana ulisema kuwa hauna pingamizi lolote.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba amesema kuwa sheria inawapa nafasi upande wa Mashtaka kusikilizwa na kupeleka maombi yao, hivyo ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 23 mwaka huu na Washtakiwa Kaburu na Aveva wamerudishwa rumande.