DC Haniu awataka Wakandarasi kuwa waadilifu

0
180

Mkuu wa wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, Jaffar Haniu amewataka Wakandarasi nchini kuwa waadilifu na kutekeleza miradi katika ubora uliokusudiwa.

Kwa upande wa waajiri, amewataka kutimiza wajibu wao kwa Wakandarasi kwa kuwalipa kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano ya mikataba, ili kupata tija iliyokusudiwa badala ya kuwalaumu kwa kuchelewesha miradi.

Haniu ametoa wito huo mkoani Mbeya alipokuwa akifunga mkutano wa siku mbili wa mashauriano ya wadau wa sekta ya ujenzi kwa mwaka 2023, kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Juma Homera.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Makandarsi nchini (CRB) Mhandisi Rhoben Nkori amesema, mkutano huo wa mashauriano ya wadau wa sekta ya ujenzi umekuwa wa manufaa katika kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kuinua sekta hiyo.

Amesema miongoni mwa maazimio waliyojiwekea ni Wakandarasi kutumia wataalam sahihi na kufuata utaratibu wanapokuwa wakifanya shughuli zao ili kuongeza ufanisi.

Maazimio mengine ni CRB ichukue hatua kali za kisheria kwa Wakandarasi wasiotekeleza majukumu yao kikamilifu, pamoja na Wakandarasi kujiunga kupitia ubia ili waweze kushindana katika miradi mikubwa na kutoa fursa kwa wanafunzi kupitia kampuni zao kujifunza kwa vitendo ili kuwaandaa wataalam wazuri wa baadae kwa ajili ya ujenzi wa Taifa.

Mkutano huo umehudhuriwa na washiriki zaidi ya 200 kutoka mikao ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ni Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma na Rukwa ambapo miongoni mwao Wakandarasi ni 183 na wasio Wakandarasi ni 20.

Mkutano mwingine unatarajiwa kufanyika jijini Arusha tarehe 03 hadi 04 mwezi Mei mwaka huu na kukutanisha wadau wa sekta ya ujenzi kutoka mikoa ya Kaskazini.