Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) wameingia makubaliano na Wakala wa Mabasi yaendayo kwa haraka (DART) katika utumiaji wa magari yaendayo haraka kurahisha usafirishaji wa wananchi ambao watakaoshiriki Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba ya mwaka 2022.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo iliyofanyika katika Ofisi za TANTRADE leo Juni 6,2022 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) Latifa Khamisi amesema katika mpango huo mfupi lengo ni kuhakikisha kunakuwa na huduma za usafiri kirahisi kwa washiriki na watembeleaji wa maonesho ya sabasaba.
Amesema wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha wanaleta kitu kipya kila mwaka wa Maonesho ya Sabasaba hivyo kwa mwaka huu wameamua kuleta suala la urahisishaji wa usafiri kwa washiriki wa Maonesho hayo.
“Washiriki wa Maonesho wataweza kuchukuliwa kutoka kituo cha Gerezani moja kwa moja na kuletwa hapa katika Maonesho ya Sabasaba, tunataka wananchi watambue kuna urahisi wa kufika na kuondoka hapa kupitia mabasi ya DART”. Amesema Latifa.
Nae Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi yaendayo kwa haraka (DART), Dkt.Edwin Muhede amesema kutakuwa na maegesho ya magari katika ameneo maalumu waliyoyaandaa ili kuondokana na msongamano wa magari kwenye sehemu moja na mengine kukosa sehemu ya kuegesha.
Amesema tiketi za kuingia katika viwanja vya maonesho zitakuwa zinapatikana pia katika vituo maalumu vya Mabasi yaendayo kwa haraka ili kuondokana na usumbufu wa kupanga foleni kusubiri tiketi katika maeneo ya Maonesho.