Daktari kikongwe atuhuhumiwa kumuua mpenzi wake kwa wivu wa mapenzi

0
269

Jeshi la polisi Mkoa wa Kigoma linamshikilia daktari wa Chama cha Msalaba Mwekundu (Red Cross) Albert Rugai (65) kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake na yeye kutaka kujiua.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Otieno amesema kuwa chanzo cha tukio hilo lililotokea Jumapili, Januari 12 mwaka huu ni wivu wa mapenzi baina yao.

Kamanda Otieno amesema kuwa mtuhumiwa huyo alimpiga kwa nyundo kichwani mara mbili mpenzi wake aliyefahamika kwa jina la Esther Kondo (42) hali iliyomsababishia majeraha makubwa kichwani, akavuja damu na ubongo kutoka nje.

Baada ya tukio hilo mtuhumiwa alijaribu kujiua kwa kunywa sumu, jaribio lililoshindikana na sasa anapatiwa matibabu na atakapopona atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili, ameongeza kamanda huyo huku akiwataka watu kutokujichukulia sheria mkononi.

“Ninawashauri wananchi waache kujichukulia sheria mkononi kama unaona mpenzi wako ana shida achana naye na utafute mwingine usijitafutie matatizo kwani huyu mzee na umri wake anaenda kufia jela.”

Kwa sasa mtuhumiwa huyo anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Kibondo ambapo pia ndipo ulipo mwili wa aliyekuwa mpenzi wake.