Corona yaingia Tanzania

0
355

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Ummy Mwalimu amethibitisha kuwepo kwa muathirika wa kwanza wa virusi vya Corona nchini Tanzania.

Mwalimu amesema kuwa muathirika ni Mtanzania mwanamke mwenye umri wa miaka 46 ambaye aliwasili nchini Machi 15 akitokea nchini Ubelgiji.

Msafiri huyu aliwasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akafanyiwa ukaguzi na kuonekana hakuwa na homa, lakini baada ya sampuli kupelekwa maabara ya Taifa. vipimo vimethibitisha kuwa ana maambukizi ya virusi vya Corona.

Aidha, Waziri Ummy Mwalimu amesema kuwa mgonjwa huyo anaendelea vizuri na matibabu.

Wakati huo huo, amesema kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti, na pia amewasihi wananchi kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo kama ambavyo wamekuwa wakipatiwa elimu.

Miongoni mwa mambo aliyoshauri wananchi kufanya ni pamoja na kusitisha safari zisizo za lazima, kuwekwa vifaa vya kunawia mikono kwenye maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu, pamoja na kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono.