Chuo Kikuu Ardhi kimeingia makubaliano ya miaka mitatu na Taasisi ya SUKOS kwa ajili ya kutoa elimu kwa Wananchi juu ya kukabiliana na majanga mbalimbali hapa nchini.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo imefanyika katika chuo hicho ambapo pamoja na mambo mengine taasisi hizo mbili zitashirikiana kutoa mafunzo kwa vitendo kwa Wataalamu wanaojihusisha na maafa nchini.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Profesa Evaristo Liwa amesema kuwa, makubaliano hayo yatawawezesha kama watoa taaluma ya majanga kunufaika na utaalamu kukabiliana na majanga kutoka kwa Wataalamu wa Taasisi ya SUKOS.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa SUKOS Kova Foundation, Kamishna Mstaafu wa Polisi Suleiman Kova amesema kuwa, wamefikia hatua ya kushirikiana na Chuo Kikuu Ardhi ili kuwawezesha kufikia malengo yao ya kutoa elimu kwa Watanzania wengi juu ya kukabiliana na majanga.
Chuo Kikuu Ardhi ndio chuo pekee hapa nchini kinachotoa shahada za kukabiliana na majanga ambapo kozi hiyo ilianzishwa mwaka 1999 chini ya kitengo cha Maafa kilichopo katika ofisi ya Waziri Mkuu.