Chuo cha Ufundi Arusha kimebuni helikopta itakayotumika kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo za uokoaji wakati wa majanga.
Mkufunzi wa Ufundi katika chuo hicho Injinia David Raymond amesema helikopta hiyo iko katika hatua za mwisho wa utengenezaji wake kabla ya kuanza majaribio ya kupaa angani.
Mbali na helikopta hiyo, Injinia Raymond amesema chuo hicho pia kimebuni baiskeli inayotumia umeme wa jua kwa ajili ya watu wenye ulemavu ambayo tayari imekamilika utengenezaji wake.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya uwekezaji mkubwa katika chuo hicho ikiwemo ununuzi wa vifaa vya kisasa katika karakana za utengenezaji vipuri vya magari, karakana ya uyeyushaji vyuma na maabara ya kufundishia mifumo ya magari.
Makamu mkuu wa chuo hicho Dkt. Yusuph Mhando amesema miradi mingine iliyowezeshwa na wizara ya elimu, sayansi na teknolojia chuoni hapo ni pamoja na ujenzi wa bweni la wasichana unaogharimu shilingi bilioni 1.4 na uboreshaji wa mifumo ya maji safi na taka uliogharimu shilingi milioni 765.