Chongolo: Suala la bandari CCM iko imara, iko timamu

0
301

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesisitiza kauli ya chama hicho kuitaka Serikali kuongeza kasi ya suala la uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari ili hatua za uwekezaji ziende katika hatua nyingine na Watanzania waanze kuona matokeo chanya kupitia mikataba ya utekelezaji.

Amesema suala la uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari ya Dar es Salaam ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025, huku akiwataka Wanachama na Viongozi wa CCM kuwa makini na wapinzani wa mradi huo wanaopita kupotosha Wananchi kwa sababu wanahofia iwapo CCM ikitekeleza kwa ufanisi kila ilichoahidi kwa wananchi kupitia ilani hiyo watakosa ajenda.

Katibu Mkuu Chongolo amesema hayo alipokuwa akihutubia Wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, ukiwa ni mwendelezo wa ziara yake ambayo ameitumia kufafanua masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali kupitia Ilani ya CCM ya
mwaka 2020 – 2025, ikiwemo suala la makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai yanayolenga kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uboreshaji wa uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam.

Kauli hiyo ya Chongolo imekuja siku moja baada ya kuitoa awali wakati akihutubia Wananchi katika mkutano mwingine uliofanyika Julai 15, 2023 katika uwanja wa Rwandanzovwe, Mbeya Mjini, ambapo alisema CCM inaitaka Serikali kuharakisha suala hilo liende hatua za utekelezaji utakaoanza kutoa matokeo chanya na kuweka bayana kuwa kazi ya kujibishana na wanasiasa wanapotosha wananchi itafanywa na chama hicho kwa sababu ndicho kiliomba na kikapewa dhamana ya kushika dola, kuunda Serikali na kuongoza nchi.

Amesema kinachofanyika ni utekelezaji kwa vitendo wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi na sio vinginevyo, huku akiwataka wanachama wa CCM kuwa makini na watu wanaokwepa kujadili utekelezaji wa ilani hiyo badala yake wanazusha maneno na kufanya siasa za kutaka kuwachonganisha na viongozi wao.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamana ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, anaongoza njia…anaongoza wanaCCM, lakini yote ni makubaliano na maagizo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na si vinginevyo. Wapo watu wanahangaika, wanatumia nguvu kubwa sana, kuhamisha masuala ya msingi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwenda kwa mtu, kumfanya aonekane Rais anayafanya yeye kama yeye. Hao watu ni wachonganishi. Ni wazushi. Wanatengeneza mazingira ya kuwagombanisha ninyi, ilani yenu, na kiongozi wenu na viongozi wenu waliopewa dhamana ya kuratibu utekelezaji wa Ilani,” amesema Chongolo

Ameongeza kuwa wapo watu wanahangaika kuhamisha ajenda, ikiwa ni mbinu ya kuwafanya baadhi ya Wanachama CCM wasione kuwa kinachoenda kutekelezwa katika suala la uwekezaji wa kuboresha utendaji wa bandari ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, ambacho ndicho chama kilichopewa dhamana ya kuongoza nchi na uwekezaji huo hatimaye utakuwa na manufaa makubwa kwa Watanzania na nchi nzima kwa ujumla.

Katibu Mkuu Chongolo amesisitiza kuwa CCM iko imara na timamu katika kusimamia utekelezaji wa masuala yote iliyoahidi kwa wananchi, huku akiwataka Wanachama na viongozi wa CCM kuisoma ilani kwa makini na kuwaelimisha wengine ili waache kukubaliana na mambo rahisi yanayotengenezwa ili kuwachonganisha.