Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameshiriki kupiga kura katika shina namba tano kata ya Kilimani mkoani Dodoma, na kuzindua shina la wakereketwa la madereva wa bodaboda na bajaji.
Aidha, amewaahidi madereva hao 26 kuwa ndani ya wiki mbili atazungumza na Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Samia Suluhu Hassan ili awape bodaboda kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Chongolo amewapongeza vijana hao kwa uamuzi wa kuanzisha tawi hilo huku akiwasisitiza kuwa litumike kwa kazi iliyokusudiwa si vinginevyo.
“Lengo letu muwe na makazi bora nyinyi na familia zetu, hivyo nawaahidi nitamuomba Rais Samia awachangie bodaboda hesabu ya jioni itakayopatikana ni yenu mtagawana,” amesema Chongolo
Aidha, Chongolo amewaagiza Viongozi wa mkoa wa Dodoma kwenda kuangalia kama Vijana hao wanakopesheka, ili wawaingize kwenye mikopo ya halmashauri.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amewasisitiza madereva hao ambao ni vijana kutumia shina hilo vizuri.
Kuhusu mikopo kwa vijana hao, Shekimweri amewataka kuunda kikundi na kukisajili lengo likiwa ni kukiwezesha kupata mikopo, na kuahidi kuwapa kipaumbele pindi watakapokamilisha shatri hilo.
Katika uchaguzi uliofanyika kwenye shina namba tano lililopo Kata ya Kilimani ambao Katibu Mkuu ameshiriki na kupiga kura, Juma Saigwa ameibuka kidedea nafasi ya Mwenyekiti kwa kupata kura 45 sawa na asilimia 90 ya kura zote zilizopigwa.
Aidha, nafasi ya Katibu imechukuliwa na Maxmillian Mtabekwa na wajumbe watatu waliochaguliwa ni Liana Danford, Regina Kalindo na John Msalika.