Chongolo : Agenda ya bandari ni ya CCM, sio ya mtu

0
134

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo @daniel_godfrey_chongolo amewataka Watanzania wasikubali kupotoshwa kuhusu mkataba wa bandari.

Amesema mkataba huo ni wa CCM na sio wa mtu mmoja, huku akisisitiza kuwa suala hilo lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 Ibara ya 59 ukurasa wa 92 kuhusu uboreshaji wa bandari.

Chongolo amesema hayo wakati akihutibia Wananchi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.

“Serikali imepewa msukumo na chama kinasimamia kuhakikisha utekelezaji unafanyika, naagiza Serikali ichakate haraka kuelekea kwenye mkataba wa uwekezaji wa bandari,” amesema Chongolo na kuongeza;

“Kazi ya maneno ya siasa ni ya wanasiasa, watendaji wasihangaike kujibu. Eti Jambo la flani hata angekuwa nani ndani ya CCM agenda isiyo na maslahi ya watu haitapita,”

Amesema ilani hiyo ya CCM ndiyo iliyoweka ahadi ya kuboresha bandari zote nchini.

“Aliyeandaa ilani ndiye aliyeweka haya malengo, mjadala wa Ilani ulianza mwaka 2020. Tuliahidi, baada kuahidi tunatekeleza. Tukicheka na wanaopotosha adhabu itakuwa kwetu,” amesema Chongolo.

Amesema CCM itakusanya maoni ya Wananchi na yale yenye tija yatafanyiwa kazi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa CCM, takwimu zinaonesha kuwa bandari kwa sasa inaingiza zaidi ya shilingi Trilioni 7 huku asilimia 99 ya fedha hizo ikitumika kwa matumizi yao wenyewe.

“Nani anakula hizo Trilionii Saba?, sasa wakiambiwa ulaji unakatwa watafunga midomo?, Kuna genge la watu wanamlo na hawataki kuona mambo yanabadilika,” amesema Chongolo na kuongeza;

“CCM tuna akili timamu na habari yao wataipata tija ikipatikana. Msikubali, msiyumbishwe agenda ni ya CCM sio ya mtu.”

Chongolo amesema hawezi kusimama na kutetea jambo ambalo haoni tija kwa Watanzania na kwamba ikiwa kuna mwana CCM hajasimama kupigania suala hilo lazima kunamashaka na uana CCM wake na sio vinginevyo.