Amiri Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli amemshukuru Rais Xi Jinping wa China kwa kuendeleza ushirikiano mzuri na Tanzania ikiwemo misaada na uwekezaji ambayo China imekua ikitoa.
Rais Magufuli ametoa shukrani hizo jijini Dar es salaam hii leo katika hafla ya makabidhiano ya magari Arobaini kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China (PLA) kwenda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyofanyika katika Makao Makuu ya JWTZ Upanga.
Amesema kuwa, pamoja kuisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii, ulinzi na usalama na miundombinu, China ndio nchi inayoongoza kwa uwekezaji hapa nchini ikiwa na miradi 723 yenye thamani ya takribani Shilingi Trilioni 13.581 na iliyozalisha ajira 87,126.
Ametaka uhusiano huo uimarishwe zaidi kwa JWTZ na PLA kujenga kiwanda kikubwa chenye uwezo wa kubangua tani Laki Mbili za korosho kwa mwaka, jambo ambalo litasaidia kuongeza thamani ya korosho za Wakulima wa Tanzania na kupelekwa China ambako kuna mahitaji makubwa ya korosho.
Amemuomba Luteni Jenerali Shao Yuanming aliyeiwakilisha PLA katika makabidhiano ya magari hayo na Balozi wa China hapa nchini Wang Ke kufikisha shukrani zake kwa Rais Xi Jinping kwa kuuendeleza na kuukuza zaidi uhusiano mzuri wa Tanzania na China na pia kufikisha ombi la kujengwa kwa kiwanda hicho.
Ameishukuru China kwa kutoa msaada wa magari hayo Arobaini kwa JWTZ ambayo amesema yataimarisha utendaji kazi wa jeshi hilo na pia ameomba PLA isaidie upatikanaji wa ndege kubwa za kubebea Askari na vifaa kwa ajili ya jeshi hilo.
“Makabidhiano haya ya magari 40 ni kielelezo kingine tena cha uhusiano wa karibu, kidugu na kirafiki uliopo kati ya Mataifa yetu mawili, tunaishukuru sana China kwa misaada mbalimbali iliyoitoa kwa Tanzania, China imekuwa mdau mkubwa wa biashara kwa nchi yetu na pia inasaidia katika utalii, kwa mfano mwaka huu tunatarajia kupata watalii 10,000 kutoka China”, amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Luteni Jenerali Shao Yuanming amemshukuru Rais Magufuli kwa kuhudhuria tukio hilo na kwa kuundeleza na kuukuza uhusiano wa Tanzania na China ukiwemo uhusiano wa kijeshi na ameahidi kuwa PLA itaendelea kushirikiana kwa ukaribu na JWTZ.
Nae Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo ametaja baadhi ya maeneo ambayo JWTZ imenufaika kutokana na ushirikiano wake mzuri na PLA kuwa ni pamoja na kujengwa kwa Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi huko Mapinga wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kilichogharimu Shilingi Bilioni 67, ukarabati na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Ngerengere uliogharimu Shilingi Bilioni 137.63, ujenzi wa awamu ya Pili ya Chuo cha Ulinzi wa Taifa mkoani Dar es salaam (NDC) utakaogharimu Shilingi Bilioni 57 na kwamba kwa sasa PLA inakamilisha maandalizi ya kujenga Makao Makuu ya JWTZ mkoani Dodoma na kushirikiana na JWTZ katika zoezi kubwa la kijeshi litakalofanyika hapa nchini kwa lengo la kubadilishana ujuzi katika ulinzi na usalama.
Amemuomba Luteni Jenerali Shao Yuanming kufikisha shukrani za JWTZ kwa uongozi wa juu wa PLA kwa msaada wa magari hayo Arobaini na misaada mingine inayotokana na ushirikiano wa majeshi hayo.
Pia, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuagiza JWTZ ipatiwe magari makubwa 12 yaliyokuwa yakitumiwa na Bodi ya Dawa (MSD) ili yasaidie shughuli zake.