Serikali ya China imeahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kuboresha sekta ya utumishi wa umma hapa nchini.
Akizungumza wakati wa Mhadhara kuhusu namna Sekta ya Utumishi wa Umma nchini China ilivyochangia maendeleo ya nchi hiyo leo Jijini Dar es Salaam leo katika Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) tawi la Dar es Salaam Balozi wa Jamhuri ya watu wa China, Wang Ke amesema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi.
Aliahidi nchi yake kuendelea kushrikiana na Tanzania katika kuboresha sekta hiyo ya utumshi wa umma.
Aidha alikabidhi Kompyuta mpakato 20 ili ziweze kusaidia maendeleo ya elimu katika chuo hicho.
Balozi Wang Ke, alisema Serikali ya China imepiga hatua kubwa kimaendeleo kutokana na watumishi wake kutumia Teknolojia ya kisasa kama Kompyuta na zana nyinginezo.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika, aliishukuru serikali ya china kwa ushirikiano wake na Tanzania na akaomba ushirikiano huo undelee.
Mkuchika alimwomba Balozi huyo kusaidia ujenzi wa Makao Makuu ya Chuo Cha Utumishi wa Umma Jijini Dodoma.
Alisema kwa sasa hivi serikali imehamia Dodoma, hivyo ujenzi wa chuo hicho jijini humo ni muhimu.
Awali Mkuu wa Chuo hicho Dr. Henry Mambo, alimwomba balozi huyo kutoa nafasi kwa baadhi ya watumishi waende nchini China kwa ajili ya kupata mafunzo mbalimbali ili kuongeza ufanisi na utendaji kazi Serikalini.
Alisema vifaa wa walivyopata vitasaidia kuwajengea uwezo watumishi wa Umma pamoja na wanafunzi wote kwa sababu kuna umuhimu wa kila mtumishi kuelewa matumizi ya Teknolojia katika maisha ya sasa na baadae.