CCM yaridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya Kimkakati

0
178

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka, amesema chama hicho kinaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati inavyoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Shaka ameyasema hayo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja jipya la Wami ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 89.02 na zaidi ya Shilingi bilioni 75 zimepangwa kutumika.

Aidha amesema jambo la kufurahisha ni kwamba ujenzi wa daraja hilo unakwenda kuandika historia ya kuwa miongoni mwa miradi michache nchini iliyokamilika kabla ya muda uliopangwa.

“Wakati Rais Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani kulikuwa na maneno mengi sana kuhusu daraja hili la Wami na si hili tu bali maneno yalikuwa mengi Rais Samia hataendeleza mirad hii ya kimkakati, wiki mbili zilizopita tulikuwa Mwanza, tumeona ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi unavyokwenda kwa kasi kuliko tunavyofikiria. Tumeona ujenzi wa meli MV. Mwanza unavyokwenda kwa kasi kuliko tunavyofikiria na leo niko hapa daraja la Wami nashuhudia kwa macho yangu, mikono yangu lakini ukisimama hapa ukiangalia kule mbele unaona namna gani ambavyo Pwani na Tanga inavyong’ara kupitia daraja hili,”- amesema Shaka.

Ameongeza kuwa, fedha zote zimetoka kwa wakati na hivyo ukichukua asilimia 47 na asilimia 42.2 unapata asilimia 89.2 kati ya hizo kazi kubwa imefanyika katika kipindi cha mwaka mmoja na miezi kadhaa ya Rais Samia Suluhu Hassan huku akieleza kwamba hapo ndipo unaona namna gani ambavyo Watanzania wananufaika na kodi zao kwa sababu fedha iliyotoka kwenye daraja hilo ni ya ndani.

“Hakuna fedha ya mjomba hakuna fedha ya msaada ni fedha ya watoka jasho wa Tanzania ndio imefanya kazi hii na mtaalamu alikuwa ananiambia katika historia ya nchi yetu na mimi nimefuatilia iko hivyo, hili litakuwa daraja la kwanza kukamilika kabla ya wakati uliokadiriwa, daraja hili lilikadiriwa litumie miaka minne lakini tutalifungua kabla ya Novemba ambao tungetegemea kwamba ndio mwezi wa mwisho,”- ameongeza Shaka.