CCM yalaani Kitendo cha Catherine na wenzake

0
201

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimechukizwa na kulaani kitendo kilichofanywa na baadhi ya Viongozi wa  Umoja wa Wanawake wa chama hicho mkoa wa Arusha wakiongozwa na mbunge wa viti maalum kupitia chama hicho Catherine Magige.

Inadaiwa kuwa Mbunge Catherine Magige na wenzake jana tarehe 27 walikwenda makaburini yalikokuwa yakifanyika mazishi ya mfanyabiashara Kuzula Madoda anayedaiwa kuwa ni mchumba wake, kitendo kilichoibua hali ya sintofahamu kutokana na watu aliokuwa nao kuvunja geti na kuingia katika makaburi hayo ya familia.

Taarifa ya CCM iliyotolewa na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka imeeleza kuwa,  chama hicho kinaheshimu katika kujenga uimara wa familia, kuheshimiana ndani ya jamii na kuendeleza upendo katika familia halali badala ya mivutano na uvurugaji usiokuwa na sababu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Shaka, CCM inatafakari na kuchunguza kwa kina kuhusu kitendo hicho, ili kuchukua hatua za kimaadili kwa wote watakaothibitika kuwa sehemu ya matukio yaliyojenga ukiukwaji wa katiba, kanuni na utamaduni wa kuheshimu na kuheshimiana uliojengeka ndani ya CCM.

Madoda, anayedaiwa kuwa ni mchumba wa Mbunge Catherine Magige, amefariki dunia Mei 24 mwaka huu na ameacha mke ambaye ni Aziza  Msuya pamoja na watoto.