CCM yaingilia kati upatikanaji mbolea ya ruzuku

0
409

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameitaka wizara ya Fedha na Mipango pamoja na wizara ya Kilimo kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa mbolea ya ruzuku kwa Wakulima nchini ili kudhibiti upandaji wa bei.

Chongolo ameyasema hayo baada ya kutembelea kiwanda cha mbolea ya asili cha Itracom, kilichopo katika eneo la viwanda Nala jijini Dodoma, ambacho kinajengwa na mwekezaji kutoka nchini Burundi.

Amesema hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan aligawa vitendea kazi kwa maofisa ugani na kuagiza wizara ya Fedha na Mipango na wizara ya Kilimo kukaa pamoja ili kuhakikisha jambo hilo linatekelezeka, hivyo ni vema likatekelezwa.

Katibu Mkuu huyo wa CCM amesisitiza kuwa ruzuku hiyo inayokwenda kuwekwa katika mbolea ni lazima iwe yenye tija na yenye kulinda wawekezaji wa ndani ya nchi.

Ujenzi wa kiwanda hicho cha mbolea ya asili cha Itracom ulianza mwezi Julai mwaka 202, na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu ambapo kwa sasa umefikia asilimia 80.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira elfu tatu na kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani laki sita za mbolea kwa mwaka.

Chongolo pia amezitaka baadhi ya taasisi na kampuni za Serikali zinazohusika kusimamia mbolea kuacha kufanya kazi kwa mazoea, na badala yake zifanye kwa ushindani katika kuratibu na kusimamia bei ya mbolea.