Bweni lateketea kwa moto

0
161

Bweni la shule ya sekondari ya wasichana Mkuza iliyopo wilayani Kibaha mkoani Pwani limeteketea kwa moto, likiwa na vifaa mbalimbali vya wanafunzi.

Tukio hilo limetokea jana usiku, ambapo mali zilizoteketea kwa moto huo ni pamoja na nguo, madaftari na vitabu.

Tukio hilo limetokea wakati wanafunzi wanaotumia bweni hilo wakiwa kwenye ibada, hivyo hakuna mwanafunzi yeyote aliyedhurika.

Baada ya tukio hilo, mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alifika eneo la tukio na kuwatoa hofu wazazi na walezi wa wanaflunzi wanaosoma shuleni hapo kwa kusema kuwa, watoto wao wako salama na wameshapata mahali pa kuwahifadhi.

Tayari timu imeundwa, kuchunguza chanzo cha moto huo katika bweni hilo linalotumiwa na wanafunzi 76.

Shule ya sekondari ya wasichana Mkuza inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
Dayosisi ya Mashariki na Pwani.