Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew ameupongeza uongozi wa halmashauri ya Butiama mkoani Mara kwa kutenga shilingi milioni 80 kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi la anwani za makazi.
Naibu Waziri Kundo ametoa pongezi hizo katika kikao kazi na Viongozi na Watendaji wa Kata ya Bumangi wakati wa ziara yake ya uhamasishaji wa utekelezaji wa zoezi la anwani za Makazi, ukaguzi wa ubora wa na upatikananji wa huduma za mawasiliano ya simu na miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF).
“Naipongeza sana halmashauri ya wilaya ya Butiama kwa sababu wao wenyenye wamekubaliana wanaenda kutenga kiasi cha shilingi milioni 80 ili kwenda kuhakikisha zoezi hili la anwani za makazi na Postikodi linakamilika ndani ya muda uliopangwa.” amesema Mhandisi Kundo
Pia ameupongeza uamuzi wa Serikali wa kutenga shilingi bilioni 1.6 kwa ajili kujenga mkongo wa mawasiliano wenye urefu wa kilomita 346 kutoka Shinyanga, Bariadi, Bunda, Butiama mpaka Musoma ambao utaenda kutatua changamoto ya mawasiliano wilayani Butiama.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Posta kutoka wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Caroline Kanuti amesema, mfumo wa anwani za makazi utakapokamilikia utawezesha kiurahisi biashara mtandao, huduma za afya na zimamoto pamoja na kufikika kwa urahisi mtu mahali anapoishi.