Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha azimio la kumsamehe Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika ambaye pia ni Mbunge wa Shinyanga Mjini, – Stephen Masele aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma mbalimbali.
Bunge limefikia uamuzi huo jijini Dodoma, baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kukamilisha kazi ya kumhoji mbunge huyo na kumtia hatiani kwa makosa manne anayodaiwa kuyatenda akiwa nchini Afrika Kusini ya kudharau kiti cha Spika, kuchonganisha Mihimili ya Dola, uongo na utoro Bungeni, jambo lililokuwa likiharibu taswira ya nchi.
Awali akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Mwenyekiti wa kamati hiyo Emanuel Mwakasaka amesema kuwa Mbunge Masele amepatikana na hatia ya kutenda makosa hayo, na hivyo akaliomba Bunge limpe adhabu ya kusimamishwa kuhudhuria mikutano mitatu ya bunge ili iwe onyo kwa Wabunge na Viongozi wengine.
Baada ya Mwakasaka kuwasilisha taarifa yake, Spika wa Bunge Job Ndugai akatoa nafasi kwa Mbunge Masele kuzungumza ambaye pamoja na mambo mengine ameliomba radhi Bunge na Viongozi wote, kutokana na usumbufu uliojitikeza wakati wa mgogoro huo.
Spika Ndugai ameipongeza kamati hiyo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kazi kubwa iliyoifanya na kuliomba Bunge kumsamehe mbunge huyo.
