Mkutano wa kumi na tatu wa bunge la kumi na moja unatarajiwa kuanza kesho jijini Dodoma ambapo wabunge wateule wanne watakula kiapo cha uaminifu huku wabunge wengine waliopita bila kupingwa hivi karibuni wakisubiri kuapishwa katika mkutano wa bunge wa kumi na nne.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma Spika wa bunge Job Ndugai amesema bunge hilo litapokea na kujadili wasilisho la mpango wa taifa unaokusudiwa kutekelezwa mwaka 2019/2020.
Spika Ndugai ameongeza kuwa miswada sita ya sheria itasomwa kwa mara ya kwanza na muswada wa sheria ya huduma ndogo za fedha wa mwaka 2018 ambao utasomwa kwa mara ya kwanza na hatua zake zote baada ya kupelekwa bungeni kwa hati ya dharura kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Magufuli.
Aidha bunge hilo litapitia na kuridhia maazimio matatu ikiwa ni pamoja na azimio la kuridhia itifaki ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu kulinda hati miliki za aina mpya za mbegu za mimea, azimio la kuridhia mkataba wa kimataifa wa kuzuia matumizi ya silaha za kibaiolojia na sumu na azimio la kuridhia mkataba wa takwimu wa Afrika.