Mtaalam wa kilimo kutoka nchini brazil Profesa Pedro Castro Neto Amewaasa Maafisa ugani nchini kuwafundisha wakulima kuhusu mbinu bora pamoja na teknolojia za kisasa za kilimo ikiwemo cha zao la pamba ili waweze kuzalisha kwa tija.
Profesa Neto ametoa wito huo katika mafunzo ya kuwajengea maafisa ugani wa halmashauri za wilaya za kwimba,misungwi na magu mkoani mwanza uwezo wa namna ya kufikisha teknolojia za kilimo kwa wakulima.
Tanzania imejaaliwa kuwa na teknolojia nyingi za kilimo ikiwemo cha zao la pamba lakini changamoto iliyopo ni namna ya kuzifikisha kwa wakulima.
Hali hiyo inadaiwa kusababishwa na sababu kadhaa ikiwemo wataalam wa kilimo kutotimiza wajibu wao katika kuwapa wakulima mbinu bora za kilimo chenye tija.
Serikali ya brazil katika kuunga mkono jitihada za kuleta mapinduzi ya kilimo cha pamba nchini inatekeleza mradi wa victoria cotton ambao umewajengea maafisa ugani uwezo wa kufikisha teknolojia za kilimo cha zao hilo kwa wakulima.
Kwa upande wake,mkurugenzi wa utafiti na ubunifu katika taasisi ya utafiti wa kilimo nchini Dkt.Evelyna Lukonge amewataka maafisa ugani kutimiza wajibu wao katika kumkomboa mkulima.
Mafunzo hayo yanawashirikisha maafisa ugani kutoka halmashauri za wilaya za kwimba,magu na misungwi mkoani mwanza ambako mradi huo unaolenga kuboresha kilimo cha pamba unatekelezwa.
