Bodi ya ZSSF yavunjwa kwa ubadhirifu

0
115

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ameivunja bodi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kutokana na matumizi mabaya ya fedha.

Dkt. Mwinyi ametangaza uamuzi huo Ikulu jijini Zanzibar wakati wa hafla ya kuwaapisha Makamanda wapya aliowateua hivi karibuni kuwa Wakuu wa vikosi maalum vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema amefikia uamuzi huo baada ya kubainika kuwa, katika ya mwezi Januari na Machi mwaka huu bodi hiyo imefanya vikao zaidi ya sita na kutumia shilingi milioni 99.7.

“Najiuliza kulikuwa na dharura gani ya kufanya vikao sita ndani ya miezi mitatu, kwa kawaida bodi zinatakiwa kufanya vikao vinne kwa mwaka na ikitokea kuna dharura ndio wanaweza kukutana zaidi ya hapo lakini kuwe na dharura,” amesema Rais Dkt. Mwinyi.

Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa hatosita kuvunja bodi ambazo zimekuwa zikifanya ubadhirifu wa fedha za Serikali.

Makamanda walioapishwa hii.leo na Rais Dkt. Mwinyi ni pamoja na Kanali Azana Hassan Msingiri aliyeapishwa kuwa Mkuu wa Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), Kanali Makame Abdallah Daima kuwa Mkuu wa Kikosi cha Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), na Kanali Rashid Mzee Abdallah kuwa Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji.

Rais Dkt. Mwinyi amewataka Makamanda hao kwenda kujenga na kurudisha nidhamu katika vikosi hivyo vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.