Serikali imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 8.5 kwa ajili ya utafiti wa kina wa Jiosayansi kuhusu rasilimali za madini ya dhahabu nchini ili wachimbaji wadogo waondokane na dhana ya kuchimba kwa kubahatisha.
Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amesema hayo katika ufunguzi wa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa eneo la Katente wilayani Bukombe mkoani Geita ambapo amesema pindi tafiti hizo zitakapokamilika watapewa wachimbaji wadogo sehemu mbalimbali nchini.
Ameeleza kuwa wachimbaji hao watakuwa na uhakika na shughuli zao za uchimbaji na namna watakavyoendelea kunufaika na rasilimali hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini nchini Mhandisi Sylvester Ghuliku amesema serikali iliwapa jukumu la kufanya utafiti pamoja na wakala wa jiolojia nchini katika vituo mbalimbali nchini ambapo Katente ni moja ya vituo hivyo.