Bilioni 4 zatumika ujenzi wa hospitali Mbarali

0
111

Jumla ya Shilingi Bilioni 4 zimetumika katika ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Kukamilika kwa ujenzi huo kumesaidia Wananchi wa Mbarali na maeneo jirani kupata huduma ya uhakika ya matibabu.

Akizungumza kuhusu ujenzi wa hospitali hiyo Mganga Mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Mbarali Dkt.Isaac Kyando amesema, kwa sasa hospitali hiyo ni kubwa na kujengwa kwa wodi kubwa ya Mama na Mtoto kumesaidia huduma kuwa salama na ya uhakika.

“Kwa sasa kwa kweli hospitali hii ni kubwa na ukiangalia jengo letu la Martenity [jengo la wazazi] ni jengo ambalo linatusaidia sana, kwa sasa kulingana na sisi hospitali ya wilaya yetu inazalisha akina mama wengi sana ambapo kwa siku tunazalisha kumi hadi kumi na tano ambapo kwa mwezi tunazalisha wamama mia nne mpaka mia tano,”Amesema Dkt. Kyando.

Kwa upande wake Muuguzi wa hospitali hiyo Yeya Adamu amesema wanaishukuru Serikali kwa kukamilisha ujenzi wa jengo jipya la hospitali ya wilaya ambapo zamani kulikuwa na ufinyu wa nafasi kwenye jengo la wazazi.

“Zamani tulikuwa kidogo na ufinyu wa nafasi ya wagonjwa lakini kwa sasa nafasi ni kubwa tunafanya kazi kwa urahisi tofauti na kule mwanzo na pia tunashukuru kwa vifaa ambavyo tumeweza kuongezewa vya kuweza kuwasaidia wamama hasa wale wamama wanaopata Watoto Njiti tumeweza kupata vifaa ambavyo vinaweza kusaidia kazi zetu,”amesema Yeya.

Naye Afisa Huduma kwa Wateja kutoka Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Mbeya, Frank Apolnary amesema wanahakikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana katika hospitali ya wilaya ya Mbarali kulingana na mahitaji yao.