Ufaransa kupitia Shirika lake la maendeleo la Ufaransa (AFD), imeipatia Tanzania mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya Euro milioni 130 sawa na shilingi bilioni 361.7, kwa ajili ya kugharamia mradi wa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme wa jua.
Mkataba wa makubaliano ya msaada huo umesainiwa jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Ufaransa nchini Frederic Clavier pamoja na Mkurugenzi mkazi wa AFD Stepanie Mouen Essombe kwa niaba ya Serikali ya Ufaransa.
Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa mkataba huo, Tutuba amesema mkopo huo utatumika kujenga mitambo ya kuzalisha umeme jua kiasi cha Megawati 50 katika wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
“Ni matumiani yangu kwamba AFD wataridhia kutupatia fedha kwa ajili ya kutekeleza awamu ya pili ya mradi huo iliyopangwa kuzalisha Megawati nyingine 100 ili kuweza kufikia kiwango cha uzalishaji kilichokusudiwa cha Megawati 150.” amesisitiza Tutuba.
Amesema AFD imetoa pia msaada wa Euro milioni 7 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa mradi huo ambao utekelezaji wake utaanza mwezi Machi mwaka 2022 hadi mwezi Machi mwaka 2023.
Tutuba ameishukuru Ufaransa kwa kuipatia Tanzania mkopo huo ambao utasaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine nchini.
Kwa upande wake Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Frederic Clavier amesema kuwa Serikali ya nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha Mpango wa Taifa wa Tatu wa Maendeleo wa miaka mitano (2021/2022 – 2025/2026 unafikia malengo yake.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaifanya Tanzania kushika nafasi ya pili kwa ukubwa Afrika Mashariki katika uzalishaji wa umeme wa nguvu ya jua na kulifanya Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuwa na umeme wa uhakika kutoka katika chanzo rafiki wa mazingira.