Serikali imeongeza zaidi ya Shilingi billion 300 katika mradi wa usambazaji wa umeme vijijini kutoka shilingi trillioni 1.5 lengo ikiwa ni kuongeza kilomita mbili za usambazaji wa umeme kila kijiji nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nishati Wakili Stephen Byabato alipokuwa katika ziara ya kukagua na kuwasha umeme katika jimbo la Msalala Wilayani Kahama Mkoani Shiyanga ambapo kwa jimbo la Msalala pekee zaidi ya shilingi bilioni 18 zimetengwa ili kukamilisha miradi ya umeme jimboni hapo.
Byabato amesema kuwa ifikapo Desemba 2023 Vijiji vyote nchini vitakuwa vimefikiwa na huduma ya Umeme.
“Pamoja na kuwasha Umeme kwenye vijiji hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Nishati, ifakapo Desemba 2023 itahakikisha kuwa vijji vyote nchini ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo vinapata umeme wa uhakika” amesema Byabato
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Msalala Iddi Kassim, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kufikisha Umeme katika vijiji hivyo na kusema kuwa umeme huo utaongeza fursa kwa Wananchi katika utekelezaji wa shughuli Mbalimbali za Maendeleo.
Pia, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kukubali kuongeza nguzo 40 kwa Kila Kijiji cha Butondolo, Mhama na Igombe ili kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme katika Vijiji hivyo.