Bilioni 3 za UVIKO zashusha neema Handeni

0
367

Mkuu wa wilaya ya Handeni mkoani Tanga Siriel Mchembe amesema upatikanaji vyumba vya madarasa 128 vya UVIKO – 19 wilayani humo, umesaidia kutatua changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta elimu.

Akizunguza na watangazaji wa kipindi cha Mirindimo kinachotangazwa na kituo cha redio cha TBC Taifa waliotembelea wilaya hiyo kuona namna Wafugaji na Wakulima walivyonufaika na fedha za UVIKO – 19, Mchembe amesema kupatikana kwa vyumba hivyo vya madarasa kutainua kiwango cha elimu kwa kuwa watoto wengi watavutika kwenda shule kutokana na uwepo wa mazingira bora ya kujisomea.

Ameongeza kuwa fedha hizo pia zimewezesha kupatikana kwa manteki ya kuvunia maji kwa ajili ya Wanafunzi shuleni, na katika kuhifadhi mazingira.

Mkuu wa shule shikizi ya Msufini ambayo ni moja ya shule zilizonufaika na fedha za UVIKO -19 Mosses Katto amesema kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo iliyojengwa kwa shilingi milioni 40, kutapunguza idadi ya watoto wa Wafugaji na Wakulima ambao walikua hawaendi shule hapo awali.

Kwa upande wake Mchumi wa halmashauri ya wilaya ya Handeni Japhet Machumu amesema kwa kutumia fedha za UVIKO 19, halmashauri hiyo imeweza kujenga vyumba vya madarasa 72 vya shule za Sekondari huku 19 vikiwa ni vya shule shikizi.

Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Handeni waliohojiwa katika kipindi cha Mirindimo wameishukuru Serikali kwa kusogeza elimu karibu na watoto wao, hali itakayosaidia kupunguza idadi ya watoto wasiojua kusoma kwenye jamii ya Wakulima na Wafugaji.