Bil 26 zapelekwa kwenye vivuko Kanda ya Ziwa

0
262

Kukamilika kwa ujenzi wa vivuko vipya vinne na ukarabati wa vivuko vinne vitakavyotoa huduma katika maeneo mbalimbali ya Ziwa Victoria, kutapunguza changamoto za usafiri kwa Wananchi wanaoishi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Hayo yamesemwa mkoani Mwanza na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, alipokagua karakana ya ujenzi wa meli na vivuko ya Songoro na kupata taarifa ya maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa vivuko hivyo vitavyogharimu shilingi Bilioni 26.

“Nimekagua na nimeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa vivuko vipya lakini pia na ukarabati wa vivuko unaoendelea, nimatumaini yangu vivuko hivi vitakamilika ndani ya muda kwani kuna baadhi ya maeneo vivuko hivyo havipo au kimebakia kimoja na hivyo kutokidhi mahitaji ya wananchi.” Amesema Kasekenya

Amefafanua kuwa kwa sasa ujenzi na ukarabati wa vivuko hivyo unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu.

Mhandisi Kasekenya amevitaja vivuko vinavyojengwa kuwa ni Kisorya – Rugezi (Ukerewe – Mwanza), Ijinga – Kahangala (Magu – Mwanza), Bwiro – Bukondo (Ukerewe – Mwanza) na Nyakalilo – Kome (Buchosa – Mwanza).

Vivuko vinavyokarabatiwa ni MV Misungwi (Kigongo-Busisi), MV Mara (Iramba – Majita), MV Ujenzi (Kisorya – Rugezi) na MV Nyerere (Bugolora – Ukara).