Bil 223 zaing’arisha Tunduru

0
166

Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imepokea
shilingi Bilioni 223.9 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro ameeleza hayo wakati wa kongamano lililoandaliwa na wilaya hiyo kuadhimisha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita.

Mtatiro amesema miongoni mwa miradi ya kihistoria iliyotekelezwa wilayani Tunduru ni ule wa ukamilishaji wa ujenzi wa msongo mkubwa wa umeme wa Kilovoti 220 kutoka Songea hadi Tunduru wenye utefu wa kilomita 210.

Amesema mradi huo ambao umetumia
shilingi Bilioni 150 kati ya fedha yote iliyopokelewa wilayani Tunduru, utamaliza kabisa matatizo ya umeme wilayani humo na utakamilika ndani ya kipindi cha miezi 15.

Miradi mingine iliyopatiwa fedha nyingi wilayani Tunduru ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni ile inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), uwezeshaji Wananchi kiuchumi, barabara vijijini, miundombinu ya shule za msingi na sekondari, miundombinu ya sekta ya afya, miundombinu ya maji, kilimo pamoja na ushirika.