Bashungwa atoa siku 7 uchunguzi kuungua soko la Karume

0
165

Waziri wa TAMISEMI, Innocent Bashungwa ametoa siku saba kwa tume iliyoundwa kuchunguza kuungua kwa soko la Karume jijini Dar es salaam kuhakikisha imekamilisha uchunguzi wake ili wafanyabiashara hao waweze kuendelea na shughuli zao za kujitafutia kipato.

Pia Waziri Bashungwa ameagiza Wakuu wa Mikoa kote nchini kufanya tathmini ya athari za moto kwenye wilaya zote na kuleta taarifa ndani ya siku 14 ili kuwe na mipango thabiti ya kuzuia ajali za moto katika maeneo yote.

Bashungwa ametoa kauli hiyo alipofanya ziara kwenye Soko la Karume kuangalia athari ya moto huo na kutoa pole kwa wafanyabiashara walioathirika na janga hilo la moto.

Naye Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ashatu Kijaji amesema Wizara yake itashirikiana na bega kwa bega na TAMISEMI kuhakikisha kuwa wafanyabiashara hao wanarudi kwenye hali zao za kawaida.

Soko la Karume lenye wafanyabiashara zaidi ya 500 lina historia ya kukabiliwa na majanga ya moto mara kadhaa ambapo tukio la leo ni tukio la tatu kutokea katika soko hilo.