Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe ametoa rai kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kushirikiana kuzalisha chakula kwa mpango ambao kila nchi itanufaika.
Akiwasilisha mada kuhusu Kilimo cha kisasa kama njia ya kukabiliana na upungufu wa chakula katika mkutano wa 53 wa Mabunge ya SADC (SADC PF 53) unaofanyika hapa nchini, Waziri Bashe amesema kila nchi ifanye uzalishaji wa mazao ambayo itawauzia na wengine kutokana na uimara wake wa kuzalisha zao husika.
Ametoa mfano wa uwezo wa Tanzania katika kuzalisha mahindi na mchele ukilinganisha na nchi nyingine za SADC na kusema ni vema nchi nyingine zinunue chakula hicho na Tanzania inunue mazao mengine kutoka nchi za jirani.
Waziri Bashe ameongeza kuwa kwa sasa tishio kubwa linalozikabili nchi nyingi za SADC ukiondoa Afrika Kusini ni upatikanaji wa mbegu, jambo ambalo linaweza kukwamisha jitihada za kuwa na uhakika wa chakula.
Kuhusu njia za kisasa za kuendesha kilimo, Waziri Bashe amesema Tanzania imepanga kuwa na hekta za mraba Milioni nane za kilimo cha umwagiliaji ifikapo mwaka 2030 ili kujiwekea uhakika wa kuzalisha chakula kipindi chote cha mwaka.