BASHE: Mahindi ya Tanzania ni salama kwa afya

0
223

Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema mahindi yanayotoka Tanzania yanakidhi vigezo vya kiafya kinyume na taarifa zinazosambaa kutoka Kenya.

Bashe amesema hayo usiku wa kuamkia leo, kupitia ukurasa wake wa Twitter (@HusseinBashe) na kuongeza kuwa zao hilo kutoka Tanzania linakidhi matakwa ya ndani na nje ya nchi.

“Mahindi ya Tanzania ni salama kwa matumizi ya binadamu na wanyama na yanakidhi vigezo vyote vya kikanda na kimataifa, ameandika.”

Mnamo Machi 5, 2021 Mamlaka ya Kilimo na Chakula, Kenya ilitoa taarifa ya kusitisha mara moja uingizaji wa mahindi kutoka Tanzania na Uganda kwani mahindi kutoka nchi hizo mbili yamepimwa na kuonesha kuwa na sumu zitokanazo na mazao kuliwa na fangasi (sumukuvu).

Naibu Waziri Bashe amesema kuwa wanaendelea na mazungumzo na Kenya kama wanachama wa Umoja wa Afrika Mashariki (EAC) ili kufikia maelewano mazuri.

Aidha, Bashe amesema majibu ya sampuli iliyochukuliwa na Kenya ni tofauti na majibu ya awali ya Shirika la Viwango la Kenya (KEBS).

“Biashara ni suala la hiari, wanaweza kununua au kutonunua kutoka kwetu. Kinachotusumbua sisi ni kauli ya upotoshaji ya Wizara ya Kilimo ya Kenya. Sisi Tanzania tunafanya Biashara ya Mahindi na Mataifa na taasisi za kimataifa na inaendelea,” ameongeza Bashe.

Tanzania inaendelea kuuza mahindi katika nchi za Burundi, DRC, Rwanda na Sudani Kusini.