Barabara ya Seneto Creater yafunguliwa

0
134

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Pindi Chana amewaagiza viongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), waendelee kuimarisha vikosi kazi vya ujenzi vilivyo katika maeneo yao ili viweze kufanya ukarabati wa mara kwa mara wa miundombinu ya barabara na kushughulikia kwa haraka changamoto za kuharibika kwa miundombinu hiyo pindi zinapojitokeza katika maeneo yote ya hifadhi.

Dkt. Chana ametoa agizo hilo wilayani Karatu mkoani Arusha wakati wa ufunguzi wa barabara ya Seneto Creater katika hifadhi ya Ngorongoro akieeleza kuwa ukarabati wa barabara hiyo ni muhimu na utawafanya watalii wanaotembelea hifadhi hiyo wafurahie vivutio vya utalii katika msimu huu wa wageni wengi.

Waziri Chana amewapongeza Watoa Huduma za Utalii (Tour Operators) na wadau wengine wa utalii kwa kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Tanzania The Royal tour kwa kujipanga vyema kuipokea dunia na kuizungumzia vizuri Tanzania, vivutio vyake vya utalii na fursa za uwekezaji.

”Natambua ongezeko la wageni limeleta somo kubwa la mahitaji ya maboresho ya miundombinu ya barabara hasa barabara ya kutoka geti la Loduare hadi Golini. Tunashukuru kwa kupata Fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO – 19 ambazo baadhi ya fedha hizo zilielekezwa kwenye matengenezo ya barabara hii ambayo tayari yamekamilika” Amesisitiza Balozi Dkt.Chana.

Licha ya kuipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kazi nzuri iliyofanyika ambayo italeta tija katika kupunguza gharama na kuongeza mvuto katika eneo hilo ameitaka ieendelee kuzifanyia maboresho barabara nyingine ndani ya Hifadhi hiyo.