Barabara ya Noranga – Itigi kukuza uchumi

0
197

Serikali imeanza kuunganisha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Makongorosi – Rungwa – Itigi yenye urefu wa Kilomita 25, lengo likiwa ni kukuza uchumi wa mikoa hiyo.

Hayo yamesemwa wilayani Manyoni, mkoani Singida na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya alipokagua ujenzi wa mradi huo pamoja na ujenzi wa barabara za mji wa Itigi zenye urefu wa Kilomita 10 kwa kiwango cha lami.

Kasekenya ameeleza kuwa barabara hiyo ambayo ilikuwa ikitumika miaka ya 1970 kabla ya barabara ya Tanzania na Zambia (TANZAM) haijajengwa kwa kiwango cha lami, na sasa Serikali imeona umuhimu wa kuijenga.

Amesema tayari Serikali imetoa shilingi Bilioni 29.770 kwa mkandarasi ambaye ni China Henan International Cooperation kutoka China, ili kuikamilisha ndani ya kipindi cha miezi 18.

“Abiria waliokuwa wakisafiri kwenda Mbeya, Iringa na mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini kutoka Kanda ya Ziwa walikuwa wakija na treni mpaka Itigi na kuchukuliwa na mabasi kwenda Mbeya na mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini, hivyo barabara hii ni muhimu sana kiuchumi”. Amefafanua Kasekenya