Barabara ya Matemwe hadi Muyuni yazinduliwa

0
175

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua barabara ya Matemwe hadi Muyuni yenye urefu wa Kilomita 7.58 iliyojengwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Cooperation kutoka China kwa gharama ya shilingi Bilioni 5.48, zikiwa ni mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Waziri Mkuu Majaliwa  amezindua barabara hiyo akiwa katika wilaya ya Kaskazini A, mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya kutimiza miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya uzinduzi huo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa,  uwepo wa barabara hiyo utawarahisishia Wakazi na wageni katika maeneo ya Matemwe, Mbuyu Tende hadi Muyuni na maeneo mengine ya mkoa wa Kaskazini kuondokana na adha ya usafiri waliyokuwa wakikabiliana nayo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Majaliwa amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi, kwa namna alivyoanza kutekeleza majukumu yake ya kuiongoza Zanzibar.