Barabara changamoto bandari ya Karema

0
179

Meneja wa bandari za Ziwa Tanganyika, Edward Mabula ameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 110 inayoelekea katika eneo la bandari ya kimkakati ya Karema mkoani Katavi.

Amesema hatua hiyo itaiwezesha bandari hiyo kupata mizigo ya makasha inayoelekea katika nchi jirani za Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Mabula ameyasema hayo mkoani Katavi wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa bandari hiyo ambapo tangu kukamilika kwa ujenzi wake mwezi Septemba, 2022 hadi sasa imeweza kuhudumia shehena ya mizigo inayoelekea nchi jirani tani 1, 500 na kusafirisha abiria 2, 970 kiasi kinachotajwa kuwa ni chini ya uwezo wa bandari hiyo katika kuhudumia abiria na mizigo.

Ameongeza kuwa bandari ya Karema ina uwezo wa kuhudumia shehena ya mizigo tani elfu 72 na kusafirisha abiria elfu kumi kwa mwaka lakini changamoto ya barabara inatajwa kuwa chanzo cha bandari hiyo kuhudumia mizigo chini ya uwezo wake.