Bandeji ya kieletroniki inayotibu majeraha

0
223

Wanasayansi kutoka Taasisi ya Teknolojia ya California nchini Marekani wamekuja na teknolojia ya bandeji ya kieletroniki inayoweza kutumika kutibu na kudhibiti majeraha ya muda mrefu kwa ufanisi zaidi na kwa gharama nafuu.

Kupitia chapisho la Jarida la Sayansi ya Kimaendeleo (Science Advances), kifaa hicho ni mahususi zaidi kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari ambao mara nyingi vidonda vyao huchukua muda mrefu kupona pamoja na majereha makubwa yaliyotokana na moto.

Kwa kawaida bandeji zilizozoeleka katika matumizi ya kila siku ni zile za tabaka la pamba lenye uwezo wa kufyonza, ila kwa bandeji hii ya kieletroniki imeundwa na chip za kieletroniki, sensa na tabaka lenye dawa.

Bandeji hiyo ina uwezo wa kupima viwango vya asidi au alkali katika kidonda pamoja na kiwango cha joto katika jeraha huku ikitambua maambukizi ya bakteria katika jeraha.

Bandeji hiyo inaelezwa kuwa na kazi tatu za msingi ambazo ni kutuma taarifa bila ya kutumia waya kutoka kwenye jeraha lililofungwa bandeji hiyo hadi kwenye kifaa maalum cha kupokea taarifa ambazo zinaweza kutazamwa baadae na mgongwa au daktari.

Kazi ya pili ya bandeji hiyo ni kutoa dawa iliyohifadhiwa katika bandeji hiyo na kuifikisha moja kwa moja kwenye jeraha ili kutibu uvimbe na maambukizi.

Kazi nyingine ya bandeji hiyo ni kutoa umeme mdogo wa volti ya chini na kuuelekeza kwenye jeraha, kitendo ambacho kinasaidia kukua kwa tishu na kufanikisha jeraha kupona kwa haraka.

Profesa Msaidizi wa masomo ya udakrari kutoka Taasisi ya Heritage Medical Research Wei Gao amesema, wataalamu wamethibitisha ufanisi wa bandeji hiyo kupitia majaribio yaliyofanyika kwa wanyama wadogo na kuongeza kuwa, wamejielekeza zaidi katika kuiboresha bandeji hiyo na kuifanyia majaribio kwenye majeraha makubwa zaidi na sugu kwani mazingira ya majeraha hutofautiana.