Bandari ya Tanga Mambo safi

0
139

Maboresho yaliyokuwa yakifanyika katika bandari ya Tanga ikiwa ni pamoja na upanuzi wa maeneo mbalimbali, yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 99
na hivyo kuboresha huduma zinazotolewa bandarini hapo.

Maboresho hayo katika bandari hiyo ya Tanga inayotegemewa na maeneo mbalimbali ya ukanda wa Kaskazini pamoja na nchi jirani yameigharimu Serikali zaidi ya shilingi Bilioni 429.

Watumishi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wamefika katika bandari hiyo na kujionea shughuli mbalimbali zikiendelea ikiwa ni pamoja na upakuaji wa mabomba kwa ajili ya mradi wa maji unaojengwa katika wilaya za Handeni na Korogwe kutoka kwenye meli kubwa iliyo tia nanga bandarini hapo baada ya kuongezeka kwa kina cha gati la bandari hiyo kutoka mita tatu za awali na kufikia mita 13.

Afisa Utekelezaji Mkuu wa Bandari ya Tanga, Gwakisa Mwaibuji amesema maboresho hayo yameongeza chachu ya uwajibikaji na kwamba katika kipindi cha miezi minne tayari meli kubwa nane zimetia nanga bandarini hapo huku zaidi ya shilingi Bilioni 10 zikikusanywa kutokana na ujio wa meli hizo.