Akikagua shughuli za uboreshaji wa Bandari ya Mtwara, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Mkoa wa Mtwara ni kituo cha biashara kwa Kanda ya Kusini. Amesisitiza kuwa Bandari ya Mtwara haikujengwa kwa ajili ya kujenga Mtwara pekee, bali ilijengwa kwa lengo la kufungua mikoa ya Kusini na kuwa Bandari hiyo inategemewa kutoa huduma kwa nchi jirani.
Vilevile, Rais Samia amesema kuwa kwa sasa Bandari ya Mtwara ni ya pili kwa ukubwa nchini, ikitanguliwa tu na Bandari ya Dar es Salaam. Amewataka watumishi wa Bandari kufanya kazi kwa bidii na weledi ili Bandari ya Mtwara ifikie kiwango cha Bandari ya Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa Serikali imejizatiti kuongeza bajeti ya kuboresha miundombinu ya Bandari ili kuvutia zaidi wafanyabiashara. Serikali pia imejiandaa kusafirisha korosho kupitia Bandari ya Mtwara, hivyo amewaomba wananchi wajiandae kuiunga mkono Serikali kwa kuongeza mapato yanayotokana na shughuli za Bandari.
Miradi iliyotekelezwa kama sehemu ya maboresho ya utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara ni pamoja na ujenzi wa Gati moja la Nyongeza lenye urefu wa mita 300, ujenzi wa mita ya kupima mafuta ili kuhakikisha mafuta yanayoshushwa katika Bandari yanapimwa, ujenzi wa sehemu ya kuhifadhi makasha, pamoja na ukarabati wa ghala na vifaa vya kuhudumia mizigo bandarini.