Balozi Mbarouk amuagiza Balozi wa Vatican

0
537

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) amekutana na kumuaga Balozi wa Vatican nchini Mhe. Askofu Mkuu Marek Solczyński baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi hapa nchini.

Akiongea wakati wa kumuaga Balozi wa Vatican jana jioni katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam, Balozi Mbarouk amempongeza Balozi Solczyński kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kudumisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania.

Pamoja na mambo mengine, Balozi Mbarouk amemuahidi Askofu Mkuu Solczyński kuwa Tanzania na Vatican zitaendelea kuhimiza amani na utulivu katika masuala yenye changamoto mbalimbali ili kuwezesha uwepo wa amani na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Baba Mtakatifu katika kulinda Amani na usalama duniani kote.

Kwa upande wake Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Marek Solczynski, amesema kuwa Vatican itaendelea kuimarisha mahusiano yake ya kidiplomasia na Tanzania kwa masuala yenye maslahi ya amani na utulivu pamoja na haki na utu.

“Tumeongelea masuala mbalimbali katika kukuza diplomasia yetu na tumekubaliana kwa pamoja kudumisha amani na usalama duniani ili kuweza kuchagiza maendeleo endelevu kwa pande zote mbili,” amesema Askofu Mkuu Solczynski.

Balozi wa Vatican nchini Askofu Mkuu Marek Solczyński aliwasili nchini Tanzania Julai 12, 2017.