BAKITA na BAKIZA watakiwa kutumia njia mbadala kukuza Kiswahili

0
184

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amelishauri Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) kutumia mitandao ya kijamii kukuza lugha ya Kiswahili ambayo inakuwa kwa kasi katika maeneo mbalimbali dunaini.

Makamu wa Rais ametoa ushauri huo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya Kiswahili, ambapo Wadau mbalimbali wa Kiswahili wanashiriki katika maadhimisho hayo.

Ameongeza kuwa takribani watu milioni mia moja duniani kote wanatumia lugha ya Kiswahili na idadi hiyo inaongezeka siku hadi siku.

Amesema, kutokana na idadi ya watu wanaotumia.lugha ya Kiswahili kuendelea kuongezeka, Wadau wanaoshughulika na kukuza lugha hiyo wanapaswa kuwa na mbinu mbalimbali ili kuhakikisha lugha ya Kiswahili inaendelea kukua.

“Taasisi zetu za BAKITA na BAKIZA zipewe fedha za kutosha ili ziandae machapisho na njia zingine kwa ajili ya kueneza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi yetu. Lakini pia wataalam wetu na Wadau mbalimbali waangalie njia za kidigitali ili kukitangaza Kiswahili chetu kupitia mitandao ya kijamii,” amesisitiza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Amezitaja baadhi ya nchi ambazo zimekuwa zikitumia lugha ya Kiswahili kuwa ni Ujerumani, China, Japan na Poland.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Abdallah Ulega amesema kwenye maadhimisho kama hayo imekuwa ikitolewa tuzo ya Shaaban Robert ambapo kwa mwaka huu tuzo hiyo itatolewa kwa Rais Dkt John Magufuli kwa kutambua mchango wake wa kukuza na kutangaza lugha ya Kiswahili.

“Miongoni mwa yatakayofanyika katika maadhimisho haya ni kutolewa kwa tuzo mbalimbali ikiwemo ile ya Shaaban Robert ambayo atakabidhiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli ambayo ni tuzo ya juu katika Kiswahili,”, amesema Naibu Waziri Ulega.

Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili yanafanyika jijini Dodoma na kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni Bidhaisha Kiswahili kwa maendeleo endelevu ya Tanzania.