Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imepeleka fedha nyingi Jeshi la Polisi ili kulisaidia liweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo hasa wakati wa uchaguzi.
Amesema kwa mwaka 2024 kutakuwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo amelitaka Jeshi hilo liwe makini zaidi katika maeneo yote ya nchi likisimamia haki itendeke na usalama uwepo katika uchaguzi huo pamoja na ule wa mwaka 2025.
Rais Samia ameongeza kuwa amekwishazungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Camillus Wambura kuwa atashughulikia changamoto za Jeshi hilo na amekwishapokea bajeti ya shilingi Bilioni 125.
Ameongeza kuwa atahakikisha anaipata bajeti kamili ili changamoto zote za Jeshi hilo zitatuliwe na liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
“Kwa hiyo bajeti nitaenda kuihangaikia niipate ili niwawezeshe msimame vema na mkasimamie vema chaguzi zetu.” Amesema Rais Samia
Alikuwa akizungumza mkoani Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi.