Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas amesema, uongozi wa mkoa huo hautasita kuchukua hatua kali kwa mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kuhujumu ubora wa korosho kwa wakulima.
Kanali Abbas ametoa kauli hiyo mkoani Mtwara wakati wa kufunga mafunzo kwa watunza maghala ya korosho na wasimamiaji wa ubora wa korosho kwenye maghala.
Aidha amewataka wasimamizi wa maghala na viongozi wa vyama vya ushirika mkoani Mtwara kuwa waadilifu na kuepuka kupokea korosho chafu.
Mkuu huyo wa mkoa wa Mtwara amelazimika kutoa kauli hiyo kufuatia taarifa za kuwepo kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa wakifanya jitihada za kuchafua korosho mkoani humo na maeneo mengi, hali inayotia doa korosho zinazozalishwa hapa nchini.
Msimu wa mauzo ya korosho kwa mwaka huu unatarajiwa kuanza rasmi Oktoba Mosi, ambapo minada itafanyika katika mikoa yote inayolima zao hilo.