Askofu Nkwande : Dkt. Magufuli ameacha ishara nzuri kwa Tanzania

0
252

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Renatus Nkwande amesema mchango wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzana Dkt. John Magufuli kwa nchi yake ni mkubwa,  na ni sadaka kwa Watanzania.

Akizungumza wakati wa Misa Takatifu ya mazishi ya Dkt. Magufuli inayoendelea hivi sasa katika Uwanja wa Magufuli wilayani Chato mkoani Geita. Askofu Nkwande amesema Dkt. Magufuli  ameacha alama, kumbukumbu na ishara nzuri kwa Watanzania.

Amesema katika uhai wake Dkt. Magufuli hakuchoka kuwahangaikia Watanzania hasa masikini, na aliwapenda Watanzania wote bila kuwabagua.

Ameongeza kuwa Dkt. Magufuli alipenda Watanzania wajikomboe, na alifanya mambo mengi ya kujitoa kwa maslahi ya Taifa, na kamwe hakujijali mwenyewe na watu wa familia yake.

Licha ya kubezwa na baadhi ya watu, kiongozi huyo hakujali hayo yote bali aliamua kuendelea kujitoa sadaka  kwa ajili ya Taifa lake, ameeleza askofu Nkwande.

Amewataka viongozi na Watanzania wote kuiga mfano wa kiongozi huyo ambaye pia hakusita kutaja jina na kumtegemea Mwenyezi Mungu katika mambo mbalimbali yaliyolitatiza Taifa.