Askofu Mwakyami: Tumuombe Mungu atuoneshe kiongozi jasiri na mzalendo

0
420

Zimebaki siku tatu Watanzania kushiriki katika uchaguzi mkuu wa kuwapata viongozi wa nafasi mbalimbali, jamii imekumbushwa kulinda amani na utulivu wa nchi kwa kumtanguliza Mungu.

Rai hiyo imetolewa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Gospel Messenger Tanzania E.G.M(T), Dkt. Riziki Mwakyami katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi waliomaliza darasa la saba 2020 katika Shule ya Msingi Chanzige”B”, wilayani Kisarawe katika mkoa wa Pwani.

“Katika kipindi hiki ni vyema kila mmoja wetu aingie kwenye uvungu wa moyo wake aongee na Mungu ili aweze kumuonesha kiongozi mwenye uzalendo kuliongoza Taifa,” amesema Askofu Dkt. Mwakyami.

Pia amebainisha kuwa zipo nchi nyingi zinazotamani umoja na amani iliyopo nchini ipotee ili ziweze kutamalaki hivyo amewataka Watanzania kutumia haki yao ya msingi kupiga kura kuwapata viongozi makini.

Kuhusu hatima ya elimu kwa watoto, Askofu Dkt. Mwakyami amewataka wazazi na walimu kuwa kitu kimoja katika kuwasadia watoto kukua kiroho na kiakili ili kujenga taifa lenye hofu ya Mungu.

“Ili kutokomeza ziro ni lazima wazazi na walimu wawe kitu kimoja katika makuzi na malezi ya watoto kukua kiroho na kiakili na kufikia ndoto zao.”

Nao baadhi ya wadau wa elimu wilayani humo wameupongeza uongozi wa wilaya hiyo kwa namna ilivyojidhatiti kupunguza idadi ya watoto wasiojua kusoma na kuandika kupitia mpango mkakati wa Mkuu wa Wilaya, Jokate Mwegelo wa tokomeza ziro mashuleni.