Askari waomba rushwa Lushoto kikaangoni

0
1641

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemkabidhi mkuu wa mkoa wa Tanga, – Martine Shigela orodha ya askari wa usalama barabarani wanaodaiwa kuwaomba rushwa madereva wa noah wilayani Lushoto.

Majina ya askari hao wanaodaiwa kuomba rushwa kwa madereva wa noah wanaofanya kazi ya kusafirisha abiria ndani ya wilaya ya Lushoto yamewasilishwa kwa Waziri Mkuu Majaliwa kupitia mabango, wakati Waziri Mkuu akiendelea na ziara yake mkoani Tanga.

Baada ya kumkabidhi majina hayo mkuu wa mkoa wa Tanga, Waziri Mkuu amemtaka afanye uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazowakabili askari hao na kisha awasilishe taarifa kwake leo Novemba Mosi.

Mbali ya wananchi kuwasilisha malalamiko hayo, Pia mbunge wa Lushoto, -Shaaban Shekilindi amemuomba Waziri Mkuu awasaidie kutatua kero hiyo ya askari wa usalama barabara kuwa na tabia ya kuomba rushwa.

Awali, Waziri Mkuu Majaliwa alizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Lushoto na kuwasisitiza kufanya kazi kwa bidii.

Amesema kuwa serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli haina msamaha na mtumishi wa umma asiyetaka kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia weledi.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, watumishi wa umma wanatakiwa kufanya kazi kwa kufuata maadili ya utumishi ili waweze kutimiza lengo la serikali la kuwahudumia wananchi kwa kutumia taaluma zao.